BRELA YAENDELEA KUTOA ELIMU YA USAJILI WA BIASHARA NA ALAMA ZA BIASHARA GEITA

 



Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) umetumia Maonyesho ya Teknolojia ya Madini yanayoendelea mkoani Geita kutoa elimu kwa wananchi kuhusu huduma zake, ikiwemo usajili wa kampuni, majina ya biashara, alama za biashara pamoja na usajili wa viwanda vidogo na vikubwa.

Akizungumza katika maonyesho hayo, Afisa Usajili wa BRELA, Athumani Makuka amesema uwepo wa BRELA katika maonyesho haya unalenga kuwafikishia wananchi elimu kuhusu majukumu yake na kuwawezesha kupata huduma mbalimbali kwa urahisi.

Amesema wananchi wa Mkoa wa Geita wamejitokeza kwa wingi katika banda la BRELA kupata elimu na huduma, huku baadhi yao wakifanya usajili wa biashara na wengine kusajili alama zao za biashara.

Makuka amewataka wananchi kuendelea kutembelea banda la BRELA ili kupata huduma za usajili wa kampuni, majina ya biashara na alama za biashara, akisema huduma hizo zinapatikana kwa gharama nafuu.

Afisa Usajili wa BRELA, Athumani Makuka

Aidha amewataka wafanyabiashara na watoa huduma ambao bado hawajasajili alama au nembo zao kufanya hivyo ili kupata ulinzi wa kisheria na kuepuka migogoro inayoweza kujitokeza kutokana na matumizi ya alama zinazofanana.

Katika hatua nyingine, Makuka amesema BRELA imeendelea kuboresha mifumo yake ya utoaji huduma kwa njia ya mtandao, ambapo mfumo wa awali wa BRELA Online Registration System umeboreshwa na sasa unatumika mfumo mpya wa BRELA Online System (BOS).

Amesema mfumo huo mpya umeboreshwa kwa lengo la kurahisisha huduma kwa wateja, kuokoa muda na kuwezesha taarifa za kampuni kupatikana kwa urahisi zaidi.


Afisa Usajili wa BRELA, Athumani Makuka akimuhudumia mwananchi

“Tupo hapa kutoa maelekezo pia jinsi ya kutumia mfumo kwa sababu ni mfumo mpya kwa wafanyabiashara, wanasheria na watu tofauti tofauti ambao wanatamani kufahamu mfumo mpya unavyofanya kazi,” alisema Makuka.

Maonyesho ya Teknolojia ya Madini yanaendelea mkoani Geita, yakihusisha taasisi mbalimbali zinazotoa huduma na elimu kwa wananchi pamoja na wadau wa sekta ya madini na biashara.

Previous Post Next Post