TANAPA YAIPONGEZA SHULE YA KADAMA ZIARA YA WANAFUNZI HIFADHI YA SERENGETI

 

Wanafunzi wa Kadama English Medium School wakiwa Hifadhi ya Taifa Serengeti 


***

Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) limeipongeza Kadama English Medium School kwa kuwapa wanafunzi fursa ya kujifunza kwa vitendo kupitia utalii wa ndani baada ya kutembelea Hifadhi ya Taifa ya Serengeti mkoani Mara. 

Ziara hiyo ya mafunzo ya wanafunzi wa darasa la saba ilifanyika Agosti 9, 2026 ikiwa ni mara ya kwanza kwa shule hiyo kuwapeleka wanafunzi kujifunza na kufanya utalii katika hifadhi hiyo maarufu nchini. 

Mwongoza watalii Shadrack Ongoa  amesema kuwa ziara za aina hiyo zina mchango mkubwa katika kuongeza uelewa wa wanafunzi kwani zinawawezesha kuona kwa vitendo mambo wanayofundishwa darasani. 

Amesema wanafunzi wanapopata nafasi ya kujifunza katika mazingira halisi huwa rahisi zaidi kuhusisha nadharia wanazofundishwa darasani na kile wanachokiona katika maisha halisi. 

Aidha Ongoa ameipongeza Kadama English Medium School kwa kuendelea kufanya vizuri katika mitihani ya kitaifa kwa zaidi ya miaka mitano mfululizo. 

Naye Mwalimu mkuu wa shule hiyo Alex  Joseph amesema kuwa ziara hizo zinawasaidia wanafunzi kuhusisha masomo wanayojifunza kwenye vitabu na mazingira halisi wanayokutana nayo wakati wa safari. 

“Ziara hizi zimekuwa na mchango mkubwa kwa wanafunzi kwa sababu wanapata nafasi ya kuona kwa vitendo kile wanachojifunza darasani.Hii huwasaidia kuelewa zaidi na kuongeza uelewa wao,” amesema. 

Ziara ya Serengeti ni sehemu ya utaratibu wa Kadama English Medium School wa kuwaandalia wanafunzi ziara za kimasomo, hatua inayolenga kuunganisha elimu ya darasani na uzoefu wa maisha halisi pamoja na kuhamasisha utalii wa ndani.

 

Previous Post Next Post