Picha: Mkuu wa Wilaya ya Geita Mhe. Hashimu Komba kutoka kushoto akiwa na Diwani wa Kata ya Ludete Mhe. Jumanne Misungwi
Geita, Julai 23, 2026; Mashindano ya soka ya MISUNGWI CUP 2026, yaliyoandaliwa na Diwani wa Kata ya Ludete, Mhe. Jumanne Misungwi, yamezinduliwa rasmi leo na Mkuu wa Wilaya ya Geita, Mhe. Hashimu Komba, katika hafla iliyovutia mamia ya wakazi kutoka maeneo ya Ludete, Geita Mjini na Katoro.
Mashindano hayo yalianza kwa mchezo
wa ufunguzi uliowakutanisha Bajaji FC na Katoro Sports Center, ambapo timu hizo
zilitoshana nguvu kwa kutoka sare ya bao 1-1 katika mchezo ulioshuhudiwa na
mashabiki wengi waliojitokeza kuunga mkono maendeleo ya michezo wilayani humo.
Awali, jumla ya timu 24 zilishiriki
hatua za mchujo, huku timu 12 zikifanikiwa kufuzu hatua ya makundi. Timu hizo
zimepangwa katika makundi manne (A, B, C na D), tayari kwa kuanza safari ya
kuwania ubingwa wa MISUNGWI CUP 2026.
Mbali na burudani ya soka, sherehe za
uzinduzi zilipambwa na michezo mbalimbali ya kijamii ikiwemo kuvuta kamba,
kukimbiza kuku, pamoja na burudani ya muziki wa kizazi kipya iliyowapa burudani
mashabiki waliohudhuria.
Akizungumza wakati wa uzinduzi, Mkuu
wa Wilaya ya Geita, Mhe. Hashimu Komba, amesema michezo ni nyenzo muhimu katika
kujenga afya bora, kuzalisha ajira kwa vijana na kuimarisha amani pamoja na
mshikamano wa wananchi.
"Nakupongeza kwa moyo wako wa kujitoa kwa jamii. Leo
umewakusanya watu wenye sifa tatu tofauti katika eneo moja kupitia
michezo,"
amesema Mhe. Komba. Ameongeza kuwa michezo ni daraja muhimu la kuunganisha jamii
na kuimarisha umoja, huku akiwahimiza wananchi kuendelea kutumia michezo kama
chombo cha kudumisha amani na maendeleo.
Kwa upande wake, mwandaaji wa
mashindano hayo na Diwani wa Kata ya Ludete, Mhe. Jumanne Misungwi, amesema
lengo la kuanzisha MISUNGWI CUP ni kutoa fursa kwa vijana kuonyesha vipaji
vyao, kujenga afya na kutumia michezo kama njia ya kujiajiri.
Aidha, ametangaza zawadi nono kwa
timu zitakazofanya vizuri katika mashindano hayo. Mshindi wa kwanza atazawadiwa
kombe, seti ya jezi, mpira pamoja na shilingi milioni 5, mshindi wa pili
atapata jezi, mpira na shilingi milioni 3, huku mshindi wa tatu akiondoka na
jezi, mpira pamoja na shilingi milioni 2.
