UCHUMI WA WANAWAKE UNAVYOLEA JAMII.

 

Ule msemo wa ukimuwezesha mwanamke umewezesha Taifa unajidhihirisha pale baada ya Kikundi cha Wanawake Jeshi Kubwa kinachopatikana katika Mamlaka ya Mji mdogo Kibaigwa Wilayani Kongwa wanaojishughulisha na shughuli mbalimbali za ujasiriamali katika kujipatia kipato na kukuza uchumi wa kaya zao na Taifa kwa ujumla kuweka akiba kila mwezi kwa ajili ya kusaidia makundi maalumu katika jamii.

 

Moja ya makundi ya wahitaji yanayopaswa kuangaliwa na kusaidiwa katika jamii ni pamoja na kundi la watoto yatima ambao wamepoteza wazazi wao wote wawili kutokana na sababu mbalimbali na kundi la watoto wanaoishi katika mazingira magumu.

 

Ni mwendo wa takribani kilomita 240 kutoka Wilaya ya Kongwa hadi Wilaya ya Kondoa ambapo kikundi hiki kimesafiri kufika katika kituo cha kulelea watoto yatima cha Alhaafidhu Islamic Orphanage Center kilichopo Kata ya Bicha Wilayani Kondoa kwa ajili ya kufanya matendo ya huruma kwa kutoa msaada kwa watoto hao ikiwa ni sehemu ya kurudisha kwa jamii sehemu ya mapato yao.

 

Bi. Shangwe Magere ambaye ni Mwenyekiti wa kikundi cha wanawake jeshi kubwa anasema kuwa kikundi hicho kina mwaka wa nne sasa tangu kuanzishwa kwake ambapo kila mwaka hutembelea vituo vya makundi yenye mahitaji ili kuwasaidia katika malezi na makuzi yao.

 

Mlezi wa kikundi Bw. Nicolas Alex anasema wameguswa na kufika kutoa msaada kwa kituo hicho baada ya kupata taarifa kuwa watoto hao hawana malazi kutokana na  changamoto ya kuunguliwa mabweni ya watoto wa kike na kiume kwa vipindi viwili tofauti hivyo wamewaletea mabati pamoja mahitaji mengine ya kimwili.

 

Kwa upande wake Mlezi na Mkurugenzi wa kituo hicho Bi. Aisha Nobe ametoa rai yake kwa jamii kuendelea kukitazama kituo hicho na kuwasaidia watoto hao dhidi ya changamoto wanazozipitia katika makuzi yao ili nao waweze kufikia malengo yao na kujenga Taifa bora la baadae.

PICHA ZAIDI




Previous Post Next Post