SHIRIKA la Umeme Tanzania (TANESCO) limewahamasisha wananchi kutumia nishati safi ya kupikia badala ya nishati chafu, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kulinda mazingira na kutekeleza sera za Serikali kuhusu matumizi bora na salama ya nishati.
Akizungumza katika shughuli hiyo, mwakilishi wa TANESCO alisema shirika hilo limejipanga kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa matumizi ya nishati safi, huku likiendelea kuja na teknolojia mbalimbali zinazoweza kurahisisha shughuli za upishi katika kaya.
Alisema TANESCO imeanza kuhamasisha matumizi ya majiko ya kisasa yanayotumia umeme, yakiwemo majiko ya pressure cooker pamoja na majiko ya teknolojia ya induction, ambayo yana lengo la kuwasaidia wananchi kuachana na matumizi ya nishati chafu.
“Lengo letu ni kuhamasisha wananchi wote waweze kutumia nishati safi badala ya kutumia nishati chafu. Kupitia mpango huu, TANESCO imekuja na majiko haya ili kuwasaidia wananchi,” alisema.
Aidha, aliwataka wananchi kutumia fursa zinazotolewa na TANESCO kupata elimu kuhusu matumizi sahihi ya umeme, nishati safi na namna ya kushiriki katika utunzaji wa mazingira, huku akisisitiza kuwa matumizi ya teknolojia hizo yanaweza pia kurahisisha shughuli za upishi majumbani.
Kwa upande wake, mmoja wa viongozi waliohudhuria shughuli hiyo aliipongeza TANESCO kwa hatua hiyo, huku akisisitiza umuhimu wa shirika hilo kuhakikisha elimu ya mazingira na matumizi sahihi ya nishati inawafikia wananchi kwa upana.
Alisema elimu hiyo haipaswi kubaki ndani ya taasisi pekee, bali wananchi wanapaswa kushirikishwa kikamilifu ili waweze kuelewa wajibu wao katika kulinda miundombinu ya umeme na mazingira.
“Naomba msihodhi nyinyi wenyewe. Kwa suala hili washirikisheni wananchi na washirikisheni vizuri. Elimu ya kutosha kwa wananchi itasaidia hata wao kutoa taarifa pale wanapoona changamoto kama nguzo inayoweza kuanguka au tatizo lingine,” alisema.
Vilevile, aliipongeza TANESCO kwa sera na mikakati inayolenga kuhakikisha maeneo yenye shughuli kubwa za uzalishaji na uchimbaji wa madini yanapewa kipaumbele katika huduma ya umeme.
Alisema hatua hiyo imeanza kuonekana katika maeneo mbalimbali na kusaidia kupunguza changamoto zinazowakabili wananchi katika upatikanaji wa huduma ya umeme.
Pia aliipongeza TANESCO kwa kuboresha mawasiliano na wananchi kupitia makundi ya mawasiliano katika maeneo mbalimbali, akisema hatua hiyo imesaidia kupunguza malalamiko na kurahisisha utatuzi wa changamoto za umeme.
Alitoa mfano wa changamoto za wananchi wanaonunua umeme lakini kukumbana na kuchelewa kwa huduma hiyo, akisema kupitia mawasiliano ya moja kwa moja changamoto hizo zimekuwa zikitatuliwa kwa haraka zaidi huku wananchi wakipatiwa elimu kuhusu matumizi ya mita na huduma za umeme.
Viongozi
hao pia waliishukuru TANESCO kwa kazi inayofanywa katika kuboresha huduma za
umeme na kuwataka wananchi kuendelea kushirikiana na shirika hilo katika
kulinda miundombinu ya umeme, mazingira na kuhamasisha matumizi ya nishati
safi.