Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Said Mtanda wa pili kutoka kushoto akikabidhi cheti cha usajili wa chama cha waandishi wa habari za pamba na mazingira kwa viongozi
MKUU wa Mkoa wa Simiyu, Said Mtanda amekabidhi rasmi cheti cha usajili wa Chama cha Waandishi wa Habari za Pamba na Mazingira (Tanzania Cotton and Environmental Journalists-TACOEJ) kilichotolewa na serikali huku akiwaahidi ushirikiano katika kuhamasisha wakulima kuongeza uzalishaji wa pamba.
Mtanda amekabidhi cheti hicho leo Nov 03, 2026 ofisini kwake mara baada ya kutembelewa na viongozi hao na kuwaahidi ushirikiano katika kuhamasisha wakulima kulima kilimo chenye tija.
Amesema kuwa atahakikisha anajifunza kwa haraka kuhusu Kilimo cha Pamba na kwamba atashirikiana na waandishi wa habari za pamba kuhamasisha wakulima wa pamba kuongeza tija ili kukuza Uchumi wa wakulima wa pamba.
"Pamba ni uti wa mgongo (backbone) wa Uchumi wa Mkoa wa Simiyu, zao hili lina changamoto nyingi sana na mimi kama mkuu wa Mkoa ninatakiwa kujifunza haraka nijue changamoto za zao la pamba." Amesema na kuongeza.
"Na tumekubaliana, pia tunayo maagizo ya serikali kufanya
vikao vya wadau kabla, ninyi mnataka kufanya kongamano, mimi naona ni
tofauti...ninyi tunatakiwa tushirikiane na Mamlaka zetu kuandaa kikao cha wadau
Kwa ajili ya zao la pamba na ninyi mtatumia kalamu zenu kiuandishi kufikisha
ujumbe mkiwa ni sehemu ya wadau wa Pamba ili yale tuliyokubaliana tuyatolee
Elimu kwa umma"
Amesema kuwa watahakikisha wanahamasisha wakulima kuongeza
uzalishaji wa pamba ili waweze kutoka kuzalisha tani 133,000 na kufikia
uzalishaji wa tani 200,000... hivyo ni lazima kufanya jitihada Kwa kushirikiana
na waandishi wa habari za Pamba na Mazingira ili jamii na umma ujue Pamba ni
kitu gani na Uchumi wa Simiyu unategemea zao la pamba.
Ameongeza kuwa atahakikisha wanashirikiana na wadau wengine wa
sekta ndogo ya Pamba na mazingira kwa kukutana mara kwa maa na kuweza kuchukua
changamoto za pamba ili ziweze kutatuliwa kwa wakati.
Katibu wa TACOEJ, Sitta Tumma aliyesimama amesema kuwa watatumia taaluma yao ya Uandishi wa
Habari kuhakikisha elimu sahihi ya kilimo cha Pamba inawafikia wakulima ili
waongeze tija katika uzalishaji.

